UFUNGUZI WA OFISI YA SIDO WILAYANI KAHAMA

Swahili

Kahama ni moja kati ya wilaya zilizoko ndani ya Mkoa wa Shinyanga na ni moja ya wilaya zinazokua kwa haraka sana katika nyanja ya uanzishaji wa viwanda vidogo, kibiashara na shughuli za uchimbaji madini. Wilaya ya Kahama inazo halmashauri za wilaya tatu ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kahama Mji, Msalala na Ushetu. Wilaya ya kahama inapatika Kusini Magharibi mwa Mkoa wa Shinyanga ikipakana na maeneo makuu manne ambayo ni Kahama game resrve Kaskazini, Ushetu upande wa kusini, Ushirombo kaskazini magharibi, Isaka Bandari kavu kusini mashariki na hifadhi ya Kigosi upande wa Magharibi.  

Jengo la uwezeshaji Wananchi kiuchumi la Kahama ni matokeo ya utekelezaji wa ziara na moja ya maagizo ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim M. Majaliwa  wakati ametembelea Wilaya ya Kahama July, 2018. Akiwa katika ziara yake ya kikazi  katika Kijiji cha Bukondamoyo kata ya Zongomela Wananchi wa Kahama walimuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwawezesha kupata huduma zifuatazo kwa karibu ili waweze kwenda na kasi ya maendeleo ya awamu ya tano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh John J. P. Magufuli.
• Kupata Ushauri na Elimu ya Ujasiriamali, Biashara na Masoko
• Kupata Elimu na huduma ya urasimishaji biashara
• Kupata huduma za fedha na usimamizi wa mikopo
• Kupata Mafunzo ya Menejimenti na usimamizi wa biashara na kilimo biashara
•  Kupata vifungashio pamoja na vifaa vingine vya kuboresha uzalishaji bidhaa kwa ubora kufikia soko
• Kupata huduma za teknolojia kwa urahisi na kuongeza uzalishaji katika viwanda vya Kahama na maeneo jirani
Katika kujibu maombi ya wananchi hao, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza Uongozi wa wilaya kutumia majengo ya iliyokuwa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mji Kahama kuwa kituo cha Uwezeshaji wananchi kiuchumi wakati akijibu maswali na maombi ya wananchi waliotaka kupatiwa huduma mbalimbali kwa karibu. Jengo hilo lilikarabatiwa mara moja na kuwatengea vyumba/ofisi wadau wa ndani na nje ya Wilaya kuanza kutoa huduma haraka iwezekavavyo kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu. Jengo hilo lilikabidhiwa kwa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kama mwangalizi mkuu na mratibu wa uendeshaji wa jengo.

Wadau muhimu waliopewa vyumba-Ofisi kwa ajili ya kutoa huduma ni pamoja na; SIDO Mkoa wa Shinyanga, TBS, PASS, VETA, TCCIA, NHIF, TRA, Tan trade, GS1 TZ ltd, NMB, CRDB, Baraza la uwezeshaji Tanzania, MKURABITA, Mfuko wa Maendeleo wa Vijana na Chuo Kikuu Huria Tanzania.