SIDO YATOA MAFUNZO YA MIKOPO KWA WAJASIRIAMALI WADOGO

Katika kuhakikisha   mikopo inayotolewa na  SIDO inatumiwa na wajasiriamali kwa kusudi lililokusudiwa, SIDO imeanza kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wake juu ya namna ya kutumia vyema mikopo waliyoomba kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza viwanda vidogo nchini. Awali, SIDO ilikuwa inatoa mikopo  kwa wajasiriamali bila kufanya ufuatiliaji endapo kusudio la mkopo limetekelezwa. Kupitia mpango mpya wa MIKOPO PLUS, SIDO inahakikisha kuwa wajasiriamali wowote wanaoomba mikopo kutoka SIDO, wanaonyesha  namna watakavyoenda kutumia  mkopo husika na wafanyakazi husika wa SIDO, nao watafuatilia kuona kama kile walichoombea kimefanyika. Kwa kufanya hivyo, mkopo uliotolewa hautawasaidia tu wajasiriamali  wenyewe bali pia serikali katika  sera ya uanzishwaji / uendelezaji wa viwanda vidogo nchini.

Kuna ushahidi  wa wazi kwamba baadhi ya wajasiriamali wamekuwa hawakidhi vigezo kwenye upataji wa  mikopo kwa sababu fulanifulani  kama vile ukosefu wa ujuzi wa ujasiriamali, kufanya uzalishaji sehemu ambazo hazistahihi, ukosefu wa kumbukumbu sahihi, ukosefu wa eneo la biashara kutokana na mazingira, kuwa na mikopo toka taasisi nyingine za fedha, ukosefu wa mdhamini wa kuaminika n.k

Hii imetokea SIDO Geita  ambapo maombi 42 ya mikopo midogo yalipokelewa na kati ya hao ni watu  7 tu waliyofanikiwa kupata mikopo ambapo 35 hawakustahili. Wale ambao hawakustahili walipatiwa mafunzo  juu ya nini cha kufanya na vigezo vya kuzingatia. Washiriki walifurahi sana kwa kuwa wengine hawakuwa kabisa na uelewa juu ya upataikanaji wa  mikopo wa SIDO na kuipongeza ofisi ya SIDO Geita kuendelea kutoa elimu hata na kwa wengine.